Jumapili: Naomi Shida: Ruthu 1:1-5
Ingawa Naomi alikuwa mfuasi mwaminifu wa Bwana, alipitia magumu makubwa. Yeye na familia yake waliteseka kutokana na athari za njaa na kulazimika kuhama kutoka nyumbani kwao. Alipoteza mumewe na wanawe wawili. Ilionekana kwamba Bwana alikuwa amemwacha na hata akamgeukia. Kama Naomi, waumini wanaweza kuwa waaminifu kwa Kristo, lakini wakapitia magumu makubwa maishani mwao; hii haimaanishi kwamba Mungu amewaacha au anawaadhibu. Wakati wa shida, Mungu anaendelea kufanya kazi kwa ajili ya mema yetu. (Warumi 8:28, 36)
Jumatatu: Naomi Anaondoka Moabu: Ruthu 1:6-13
Naomi aliwasihi wakwe zake wawili wabaki katika nchi yao wenyewe. Ujitoaji na upendo usio na ubinafsi uliokuwepo kati ya Naomi na Ruthu unatufundisha kwamba uchaji wa kweli daima hujumuisha utunzaji wa upendo na kujitolea kibinafsi kwa ajili ya wanafamilia wetu. (Waefeso 5:21-6:4)
Jumanne: Upendo Mshikamanifu wa Ruthu: Ruthu 1:14-18
Ni wazi kwamba Naomi alikuwa amemfundisha Ruthu imani yake kwa Bwana Mungu kwa mfano na mafundisho. Imani ya Ruthu kwa Mungu ilimfanya abaki mwaminifu katika upendo wake kwa Naomi. Ruthu anaonyesha kanuni ya kimungu kwamba yeyote atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. (Mathayo 10:39; Ruthu 4:13-17)
Jumatano: Naomi na Ruthu Waenda Bethlehemu: Ruthu 1:19-22
Kama mwitikio wa kawaida, Naomi alimlaumu Mungu kwa msiba wake. Naomi alikuwa anajua makosa yake mwenyewe na aliona mateso yake kama adhabu ya Mungu kwa dhambi zake mwenyewe. Kwa upande mwingine, Mungu anaona mateso kama sehemu muhimu ya kusudi lake kuu na la upendo. Mwamini anayepitia motoni anaweza kutoa harufu nzuri na ya kupendeza kwa Bwana. (Mhubiri 7:14; Zaburi 33; Isaya 43; 1 Petro 5)
Alhamisi: Majaliwa ya Mungu: Ruthu 2:1-3
Katika sheria ya Musa, Mungu alikuwa amewaamuru Waisraeli kuwaruhusu maskini na wahitaji kukusanya nafaka iliyobaki mashambani baada ya mavuno. Mungu anataka wale walio na vya kutosha kuwagawia wale walio na uhitaji. (Mambo ya Walawi 19:9; 23:22; 2 Wakorintho 8:13-15)
Ijumaa: Utoaji wa Mungu: Ruthu 2:4-16
Hata katikati ya uasi mkuu wakati wa kipindi cha waamuzi, Mungu aliwalinda wale waliomtafuta kwa uaminifu wa dhati na imani iliyojitolea. Hadithi ya Ruthu ni hadithi ya utoaji wa Mungu katika maisha ya wote wanaomtumaini na kufuata njia zake. (Zaburi 17:8; 36:7; 63:7)
Jumamosi: Ruthu Anashiriki na Naomi: Ruthu 2:17-23
Ruthu alipomshirikisha, Naomi alianza kuelewa kwamba Mungu hakumtupa na kwamba upendo na wema wake kwake viliendelea. Mtazamo wake ulibadilika kutoka kwa mtazamo wake wa awali kwamba Mungu alikuwa amemgeukia.